4 Desemba 2019 - 09:27
Rouhani: Nchi za Asia Magharibi zinapasa kuwajibika ipasavyo katika kudhamini usalama wa eneo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa nchi za eneo la Asia Magharibi zinapasa kushiriki katika kudhamini usalama wa eneo na kuwajibika ipasavyo katika uwanja huo. Amesema Iran imewasilisha Mpango wa Amani ya Hormoz kwa mtazamo huo.

(ABNA24.com) Akizungumza leo Jumanne hapa Tehran na Yusuf bin Alawi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  amesisitiza kuwa hakuna njia nyingine ghairi ya undugu na urafiki kati ya nchi na mataifa ya eneo  hili. Ameongeza kuwa hali ya usalama inapasa kudhaminiwa katika eneo hili khususan katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz na kutotoa mwanya kwa uingiliaji wa nchi ajinabi kupitia kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za eneo.

Rais Rouhani ameutaja mgogoro wa Yemen kuwa moja ya kadhia na matatizo makubwa yanayolisibu eneo hili na kueleza kuwa vita vya Yemen havijawa na matunda yoyote ghairi ya kusababisha uharibifu, watu kuuawa, kuibua chuki baina ya watu wa nchi mbili na kutishia umoja wa adhi nzima ya Yemen.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Ulaya na Marekani hazina azma ya kurejesha amani huko Yemen bali pande hizo zinafuatilia kuuza silaha zao na kwamba nchi zote zinapaswa kufanya juhudi ili kuhitimisha haraka vita huko Yemen na kurejesha amani na uthabiti nchini humo chini ya kivuli cha mazungumzo ya amani kati ya makundi  ya Wayemen.

Katika mazungumzo hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman hapa Tehran, Rais Rouhani ameashiria namna Iran isivyo na tatizo lolote la kustawisha uhusiano kati yake na jirani zake na kuangalia upya uhusiano kati yake na Saudi Arabia na kueleza kuwa: Siasa za serikali ya Saudi Arabia huko Syria, Iraq na Lebanon hazijawa na matunda kwa nchi hiyo na kwamba watawala wa nchi hiyo wanapasa kubadili mkondo wa siasa zao hizo.   

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Oman inaweza kuwa kituo kwa ajili ya biashara za Iran katika eneo na kusisitiza kuimarishwa ushirikiano kati ya nchi mbili hizi.

Katika mazungumzo hayo naye Yusuf bin Alawi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amekutaja kuimraishwa uhusiano na ushirikiano kati ya Iran na Oman kuwa ni kwa maslahi ya nchi zote za eneo hili na kuongeza kuwa: Ubunifu wa Iran katika kuwasilisha mpango wa Amani ya Hormoz bila shaka utakuwa kwa maslahi ya wote na kwa ajili ya kudumisha amani na usalama wa nchi za eneo. 

..........
340